
Dar es Salaam. Waziri wa zamani katika Serikali ya Awamu ya Tatu ya Rais Benjamin Mkapa na katika Awamu ya Nne ya Rais Jakaya Kikwete, Dk Juma Ngasongwa amesema kuwa Chama Cha Mapinduzi (CCM), kinababaika katika kutekeleza majukumu yake.
Vilevile, chama hicho kimekumbwa mgawanyiko kati ya watendaji wake na Serikali na kwamba taifa lina ombwe la uongozi.
Kutokana na hali hiyo, Dk Ngasongwa ambaye pia ni kada wa CCM amemshauri Rais Kikwete kuwa mkali katika kusimamia watendaji wake anaowateua ndani ya chama na Serikali yake na kufuatilia na kupima utekelezaji wa yanayokubaliwa .
Alikuwa akizungumza katika mahojiano maalumu na gazeti hili nyumbani kwake mkoani Morogoro anakoendesha maisha yake kwa kilimo cha mpunga baada ya kustaafu.
Dk Ngasongwa alisema kuwa mgawanyiko huo kati ya watendaji wa Serikali na CCM, umeondoa umoja siyo tu katika vyombo hivyo, bali pia miongoni mwa wabunge wa chama hicho tawala.
Alisema kuwa hali hiyo inasababisha kutokea mambo mengi ikiwamo matukio ya mawaziri kushinikizwa kujiuzulu kama ilivyotokea hivi karibuni na kwamba kwa Serikali ya Awamu ya Nne hali hiyo imekuwa ikijirudia.
“Chama tawala kinababaika sana, tena hata watendaji wa CCM, wanawasema vibaya mawaziri hadharani, wakati wote ni wateuliwa wa Rais (Jakaya Kikwete) na ndiye mwenyekiti wetu wa CCM. Hii inakigawa chama. CCM ina utaratibu wake, kwa nini wasiitwe wakahojiwa ndani ya chama, badala ya kutajana hadharani:
“Sielewi kwa nini CCM inababaika. Inachotakiwa ni kuwa na mshikamano kwa wabunge wake kukutana mara kwa mara na kujenga msimamo. Hii ni kazi ya mawaziri na wabunge pia,” alisema Dk Ngasongwa na kuongeza:
“…Tatizo uongozi haufanyi kazi vizuri, ndani ya chama chetu kuna mgawanyiko mkubwa hata katika Serikali, mfano Mwanasheria Mkuu (AG) anaposema baadhi ya mawaziri hawamsikilizi, hii ‘No’ (hapana), lazima kanuni za uendeshaji wa Serikali zifuatwe, hii ni muhimu.”
Alisema hali hiyo inaonekana hata kwenye Baraza la Mawaziri na kwamba mgawanyiko pia upo ndani ya Bunge kwa wapinzani.
“Lakini kugawanyika kwa upinzani ni afadhali kuliko CCM, kwani matokeo yake ni kupunguza imani ya watu kwa Serikali yao na chama tawala,” alisema.
SOURCE : gazeti-mwananchi


No comments:
Post a Comment