Drop Down MenusCSS Drop Down MenuPure CSS Dropdown Menu

Tuesday, 31 December 2013

Kutana na vijana walioamua kujiajiri


Watu wengi wanapenda kuwa na maisha bora, wengi wanaishia kuwa na hali duni. Baadhi ya watu wamekuwa wakijiuliza ‘kwa nini ninakuwa na maisha duni’, ingawa jibu lake ni kwamba adui wa kwanza wa maisha yako ni wewe mwenyewe…Kukata tamaa kwako.
Je, wewe unayesoma makala haya una hali gani ya maisha? Kila mtu analo jibu lake. Kwa vyovyote unavyoweza kujibu, kitu ambacho unapaswa kubaki nacho katika akili yako ni kwamba hatima ya maisha yako itatokana na matendo yako; huwezi kupanda bangi shambani mwako halafu unakatarajia kuvuna mpunga; utavuna kile ambacho unakipanda.
Tunapoelekea kuumaliza mwaka 2013 na kuingia mwaka 2014 ni suala la msingi sana kutafakari namna unavyoishi, ni lazima mwanadamu awe tofauti na mnyama, apate muda wa kujitathmini namna anavyoishi na kuona kama yuko sahihi au la, wapi ajirekebishe ili mambo yaweze kwenye mbele.
“Kati ya mambo ambayo nawaasa sana vijana na Watanzania kwa ujumla kujitazama nayo ni kuhusiana na suala zima la kipato, maisha ya wengi yanakuwa duni kwa sababu ya wao wenyewe kushindwa kuthubutu kufanya mambo. Wengine ni wepesi wa kukata tamaa,” anasema Khamis Tembo, mmoja wa viongozi katika taasisi yenye kutoa huduma mbalimbali zikiwemo za kufanya usafi.
Tembo anasema yeye na vijana wenzake waliohitimu vyuo mbalimbali nchini wamelazimika kuanzisha taasisi waliyoipa jina la TZAID; Tanzania Agency for International Development, yaani Shirika la Msaada la Watu wa Tanzania kama lilivyo lile la Watu wa Marekani (USAID), azma ni kuisaidia jamii, pia kuitangaza Tanzania nje.
“Ni kutokana na tatizo la ajira tuliona tuungane vijana kutoka katika vyuo mbalimbali, ndipo mwaka jana tukaamua kuanzisha shirika hili ambalo kwa kweli limepokelewa vizuri na watu mbalimbali nchini,” anasema Tembo ambaye ni Mkurugenzi wa Miradi katika shirika hilo.
Anasema mojawapo ya huduma ambazo zinaendeshwa ni kutoa elimu ya ujasiriamali na utengenezaji wa bidhaa mbalimbali zikiweko vyakula vya mifugo ikiwemo kuku na namna ya kuendesha ufugaji bora.
“Tunaendesha pia mafunzo kwa njia ya semina na ana kwa ana juu ya namna ya kuanzisha na kuendeleza miradi mbalimbali kwa mafanikio. Tumepokea barua kutoka kwa wabunge na viongozi kadhaa ambao wamekuwa wakitushawishi twende kwenye maeneo yao kuendesha mafunzo ya utengenezaji wa bidhaa zikiwemo sabuni, mishumaa, shampoo, mikate, batiki  na nyingine nyingi. Tulikuwa kwenye hatua nzuri za kwenda Sudani ya Kusini kwa ajili ya kuendesha mafunzo ya namna ya kutengeneza bidhaa mbalimbali kwa nchi nzima, kwa bahati mbaya hali ya usalama kwa sasa si nzuri, hata hivyo tunajipanga kuangalia  namna gani tunaweza kwenda kuendesha mafunzo hayo,” anasema Tembo.
Mwanzoni mwa mwaka huu waliamua kuanzisha mradi wa kufanya usafi hasa baada ya kupata teknolojia ya kufanya usafi kutoka Malaysia. “Tulipata msaada wa elimu ya usafi kutoka Kampuni ya Mosa inayojihusisha na teknolojia iitwayo Mosa ya usafi wa aina mbalimbali hasa ule uchafu mgumu ulioshindikana,” anafafanua Tembo.
Tangu waiingize teknolojia hiyo mpya nchini, wamepokea kazi nyingi za kufanya usafi kwenye majengo mengi nchini hasa katika Jiji la Dar es Salaam.
“Tumepokea tenda nyingi na tunashukuru kwamba kwa sababu tunao wafanyakazi wengi, haitupi shida kufanya kazi hizo, kwa sasa tunajipanga kuelekea Tanga kwa ajili ya kufanya mazungumzo na baadhi ya viongozi wa Serikali ili kuangalia namna gani tunaweza kuwasaidia katika harakati zao za kuwasaidia watu kuwa na maisha bora, kupitia kuendesha wa ujasiriamali na utengenezaji bidhaa mbalimbali,” anafafanua.
Aidha Ofisa Uhusiano wa TZAID, Robert Kidogi anasema mkakati uliopo kwa sasa ni kuzisambaza huduma zao ndani na nje ya Dar es Salaam, pamoja na nchi jirani, kwani teknolojia hasa za usafi walizonazo ni ngeni.

No comments:

Post a Comment