MHADHIRI wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Benson Bana, amesema wananchi walitarajia katika hotuba ya kuaga mwaka 2013 na kuukaribisha mwaka 2014 Rais Jakaya Kikwete angezungumzia sekta ya elimu kwa upana zaidi kwa kuwa ni sekta nyeti na muhimu.
Dk. Bana alitoa kauli hiyo alipozungumza na Tanzania Daima jana kuhusu hotuba ya rais aliyoitoa juzi.
Alisema msisitizo alioutoa kwenye elimu hautoshi, kwani sekta hiyo inahitaji kuundiwa Operesheni Okoa Elimu, lakini isiwe kama ile ya Operesheni Tokomeza Ujangili.
Alisema wananchi wameshasikia kauli za mipango mingi kuwa mbioni, hata hivyo utekelezaji wake umekuwa ukienda polepole, hivyo ni lazima kukawa na operesheni hiyo ambayo itasaidia kuokoa elimu.
“Sekta ya elimu inahitaji kufanyiwa mabadiliko ikiwemo kubadili uongozi wote, ili waje watendaji wengine wenye mawazo mapya,” alisema.
Mbunge wa Ubungo, John Mnyika, akizungumzia Operesheni Tokomeza Ujangili alisema kabla rais hajaunda tume ni lazima ayaweke hadharani matokeo ya Tume ya Haki za Binadamu kuhusu kifo cha mwandishi wa habari wa Channel Ten, Daudi Mwangosi.
Alisema hadi sasa matokeo ya tume hiyo na nyingine hayajatangazwa hadharani, hivyo kufanya tume hizo kutumia kodi za wananchi bila ya sababu za msingi.
SOURCE : Tanzania Daima


No comments:
Post a Comment