Drop Down MenusCSS Drop Down MenuPure CSS Dropdown Menu

Thursday, 23 January 2014

Mbunge Afariki Dunia


Mke wa Rais Mama Salima Kikwete akiagana na ndugu wa aliyekuwa Mbunge wa Chalinze, Marehemu Said Bwanamdogo wakati alipokwenda kuwafariji nyumbani kwa marehemu, Mbezi Makondeko, Dar es Salaam jana. Picha na Salim 
Dar es Salaam. Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limepata pigo lingine kwa kuondokewa na Mbunge wa Chalinze (CCM), Said Bwanamdogo, ambaye amefariki dunia baada ya kuugua kwa muda mrefu.
Bwanamdogo alifariki dunia jana katika wodi ya Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Upasuaji wa Mishipa ya Fahamu (Moi) alikokuwa akitibiwa.
Msemaji wa Moi, Jumaa Almasi alisema Bwanamdogo alifariki saa moja asubuhi jana na mwili wake umehifadhiwa chumba cha kuhifadhia maiti katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.
Rais Jakaya Kikwete anatarajiwa kuongoza Watanzania kesho katika mazishi ya mbunge huyo kijijini kwake Miono, Kata ya Miono wilayani Bagamoyo mkoani Pwani.
Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mwantumu Mahiza alisema kwa sasa msiba huo upo Makondeko jijini Dar es Salaam na taratibu zinafanyika kuhamishia mwili wa marehemu kijijini kwake kwa shughuli nyingine za maziko.
Akizungumza nyumbani kwa marehemu jijini Dar es Salaam, baba mdogo wa marehemu, Omar Nguya alisema kuwa mwili wa mbunge huyo utazikwa kesho kijijini hapo.
Nguya alisema kuwa kabla ya mwili wa mbunge huyo kusafirishwa, kutakuwa na shughuli ya kuaga kitaifa itakayofanyika kesho kwenye viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam.
Katika hatua nyingine, Spika wa Bunge, Anne Makinda ameeleza kusikitishwa na kifo cha Bwanamdogo.
Taarifa ya Idara ya Habari, Elimu kwa Umma na Uhusiano wa Kimataifa ilisema kuwa mipango ya mazishi inaendelea kufanywa na Ofisi ya Bunge kwa kushirikiana na familia ya marehemu.
Hali ya mbunge huyo ilianza kubadilika tangu mwaka juzi, ambapo alisafirishwa kwa matibabu zaidi nchini India.
Bwanamdogo alitibiwa huko kwa zaidi ya miezi tisa, kabla ya kurejeshwa nchini baada ya familia yake kuomba aendelee na matibabu akiwa hapa nchini. Marehemu ameacha mjane na watoto sita.
Bwanamdogo ni mbunge wa pili kufariki tangu kuanza kwa mwaka huu akimfuatia Waziri wa Fedha, Dk William Mgimwa aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Kalenga, mkoani Iringa, aliyefariki dunia Januari Mosi, katika Hospitali ya Kloof Medi-Clinic, Pretoria, Afrika Kusini ambako alikuwa amelazwa.
Wabunge wengine ambao wamefariki tangu mwaka 2010 ni pamoja na Mbunge wa Jimbo la Chambani (CUF) na Salim Hemed Khamis, Mbunge wa Viti Maalumu , Mbunge kutoka Baraza la Wawakilishi, Mussa Khamis Silim na aliyekuwa Waziri wa Fedha, Dk William Mgimwa.
JK atuma rambirambi
Kutokana na msiba huo, Rais Kikwete alimtumia salamu za rambirambi Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Anne Makinda kutokana na kifo cha mbunge huyo.
Rais Kikwete alielezea kushtushwa na taarifa za kifo hicho.
“Nimeshtushwa, nimesikitishwa na kuhuzunishwa mno na taarifa za kifo cha Mbunge wa Jimbo la Uchaguzi la Chalinze kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi, Said Ramadhan Bwanamdogo,” alisema Rais Kikwete.
“Kwa hakika kifo cha mbunge huyu ambacho kimenigusa mno, siyo tu ni pigo kubwa kwa Bunge letu la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alikokuwa akichangia kwa umahiri mijadala na hoja mbalimbali, bali pia kwa wananchi wa Jimbo la Chalinze ambao alikuwa akiwawakilisha vyema,” alisema.
Rais Kikwete katika salamu zake hizo pia amewataka wanafamilia wa Bwanamdogo kuwa wavumilivu katika kipindi cha majonzi kwa kuutambua ukweli kwamba kazi ya Mungu haina makosa.
Amewahakikishia wanafamilia, ndugu na jamaa wa marehemu Bwanamdogo kuwa katika msiba huu, hawako peke yao kwani yeye binafsi yuko pamoja nao katika kipindi chote cha maombolezo.

Imeandikwa na Aidan Mhando, Beatrice Moses, George Njogopa, Dar; na Julieth Ngarabali, Pwani.
SOURCE : mwananchi

No comments:

Post a Comment