
Mwaka huu wa 2014, uwe ni mwaka wa kujirekebisha katika uandishi kwani yako matukio mengi ya kihistoria yatakayotokea.
Matukio haya ni maandalizi ya uchaguzi mkuu ujao, kura ya maoni kuhusu Katiba Mpya, utayarishaji wa Rasimu ya Katiba ya Tanganyika, Uchaguzi wa Serikali za Mitaa na mambo kama hayo.
Kutokana na umuhimu huo, waandishi na watangazaji wa vyombo vya habari, wana wajibu mkubwa wa kuwaelimisha wananchi kwa usahihi, kutumia lugha sanifu na fasaha kuhusu matukio haya.
Jambo muhimu ni kuandika kitu chenye usahihi, bila ushabiki wa kisiasa. Pili ni kutumia msamiati rahisi na wenye kueleweka, kwani wasomaji wengi wa magazeti ni watu wenye elimu ya wastani (elimu ya msingi).
Kwa mfano wanaochanganya herufi /l/ na /r/; kwa mfano ajari na ajali au karamu na kalamu wanaupotosha umma. Ajari ni malipo kwa kazi ya ziada au ovataimu, wakati ajali ni tukio lenye madhara linalotokea ghafla.
Karamu ni vyakula na vinywaji vinavyoandaliwa watu wengi kwa shughuli maalumu. Kalamu ni kifaa kinachotumiwa kuandika kwenye karatasi.
Tunayo mifano mingi ya aina hii, ambayo waandishi, hata watangazaji wa redio na runinga wameupotosha umma kutokana na athari ya lugha za asili.
Wako wale walioathiriwa na lugha za kigeni. Wao wanachanganya maneno ya Kiswahili na ya Kiingereza, ama kwa kukosa msamiati unaofaa au kwa kujionyesha kuwa wana taaluma ya lugha ya kigeni.
Utasikia akisema: “ Leo niko bize sana na sina time ya kuja kukutembelea.” Kwa bahati nzuri, visawe vya maneno ‘bize na time’ vipo.
Kwa nini msemaji aamue kujidhalilisha kwa kuiga maneno ya kigeni ?
Mbali na kuchanganya maneno, wako watu wengine wanaoiga miundo ya kigeni.
Kwa mfano: “Nitasafiri, aidha kwa treni au kwa basi ili tukutane stesheni.” Huu ni muundo wa Kiingereza kwani aidha ilikuwa ni badala ya ‘either’ na au ni tafsiri ya ‘or’ na hivyo tunapata ‘either …or’ ingetakiwa kuandikwa ‘ama’ ‘au’.
Tatu, sentensi zinatakiwa ziwe fupi na siyo tata zenye miundo isiyoeleweka kwa urahisi. Inashauriwa kutumia alama za uandishi kama nukta, mkato, nukta mkato, n.k.
Siku chache zilizopita nilisoma aya moja ya taarifa yenye maneno 69, ambayo haikuwa na alama yoyote ya kituo kama nukta, mkato au kiulizo.
Kwa bahati nzuri, baada ya kufanya uchunguzi niligundua kuwa mwandishi alikuwa ni mhariri wa gazeti maarufu hapa nchini. Swali ni je, mhariri alishindwaje kurekebisha maandishi haya?
Natoa rai kwa waandishi na watangazaji kuwa mwaka 2014 uwe ni mwaka wa mageuzi katika uandishi na utangazaji na kauli mbiu iwe: “Mwandishi na mtangazaji ni kioo cha jamii.”
Kwa hiyo nitaendelea na juhudi za kutoa maoni na ushauri kila inapohitajika kwa kuzichunguza sentensi zilizoandikwa kwenye magazeti yetu ya kila siku. Kwa mfano:
“Yeye ndiye aliyepiga pasi hovyo ndani, lakini baada ya kuwahi kumsaidia Kavannaro, yeye akasimama.”
Matumizi ya neno hovyo, yamekosewa ijapokuwa watu wengi wanalitumia hivyo. Neno sahihi ni ovyo.
“ Mwandishi wa makala hii ni miongoni mwa waandishi tisa kutoka mataifa tisa ya Afrika walioalikwa na Ubalozi wa Sweden nchini humo kwa ziara ya mafunzo.”
Makala ni maandiko au maandishi au sehemu ya andiko kubwa.
Ni sahihi kuandika makala haya na siyo makala hii. Hutumika katika umoja na wingi. Neno makala lina misingi inayofanana nakubaliana na maneno kama maradhi, madhumuni, mahakama au maudhi. Halina umoja.
Pili, maneno ‘nchini humo’ hayana umuhimu wowote kuendelea kutumika. Maneno haya yangeweza kuachwa bila kuathiri maana iliyokusudiwa.
0754 861664 / 0716 694240
SOURCE : mwananchi
SOURCE : mwananchi
No comments:
Post a Comment