Drop Down MenusCSS Drop Down MenuPure CSS Dropdown Menu

Thursday, 23 January 2014

Wanafunzi watano wafariki dunia Mtwara

Mtwara. Wanafunzi watano wa Sekondari ya Mustapha Sabodo, Kijiji cha Msijute, Wilaya ya Mtwara Vijijini, wamekufa baada ya kugongwa na gari wakikimbia mchakamchaka eneo la shule.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara, Zelothe Stephen alisema ajali hiyo ilitokea Jumatatu asubuhi maeneo ya shule hiyo Barabara ya Mtwara-Lindi. Zelothe alisema gari hilo aina ya Mercedes Benz lilikuwa likitoka Mtwara kwenda Lindi.
Alisema waliofariki ni wanafunzi watano na 26 walijeruhiwa, walitibiwa Hospitali ya Rufani Mtwara na kuruhusiwa.
“Asubuhi ya leo (Jumatatu) saa 11:40 ajali imetokea maeneo ya Sekondari ya Mustapha Sabodo, Kijiji cha Msijute Barabara ya Mtwara- Lindi, polisi wakati huo walikuwa tayari wapo kazini na kusaidiana kutoa huduma,” alisema Zelothe.
Alisema wanamshikilia dereva wa gari hilo, ili hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa.
Aliwataja waliopoteza maisha kuwa ni Khairath Mohammed, Mwanahamis Mohammed, Asma Mpunja, Fatuma Ally na Hilda Mathias.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Mtwara, Wilman Ndile alisema ajali hiyo imesikitisha na kwamba, kwa kushirikiana na viongozi tayari ameunda kamati ikiongozwa na Mganga Mkuu wa Mtwara na maofisa elimu kuona jinsi watakavyosafirisha maiti, huku moja ikiwa inapelekwa mkoani Lindi.
“Ajali imetokea asubuhi na viongozi tumeweza kushirikiana tayari tumeunda kamati ikiongozwa mganga mkuu kuona jinsi tutakavyosafirisha maiti,” alisema Ndile.
Aliwataka wananchi kuwa watulivu hasa Kijiji cha Msijute kutokana na taarifa kuwa, walitaka kufunga barabara.
Mganga Mkuu wa Hospitali ya Rufani ya Ligula, Dk Shaibu Maarifa alikiri kupokea majeruhi na maiti zilizosababishwa za ajali hiyo.
Dk Maarifa alisema kwa kushirikiana na madaktari na vijana kutoka Chuo cha Wauguzi cha Cots, wamejipanga vizuri kukabiliana na majeruhi wa ajali hiyo.
“Ilikuwa saa 12:30 alfajiri tumepokea watu 51 kuhusiana na hiyo ajali, kati yake maiti zilikuwa tatu, wa nne amefariki wakati ameshafika hapa,” alisema Dk Maarifa.
Alisema wanafunzi 26 walitibiwa na kuruhusiwa na kwamba, majeruhi 21 wamelazwa kwa matibabu zaidi. “Majeruhi mmoja ni msichana hali yake siyo nzuri, tunafanya taratibu za kumhamisha,” alisema Dk Maarifa.
Baadhi ya wanafunzi waliojeruhiwa, Eva Issaya (14) wa kidato cha pili alisema walikuwa wamepanga mstari kwa ajili ya namba.
SOURCE : mwananchi

No comments:

Post a Comment