Drop Down MenusCSS Drop Down MenuPure CSS Dropdown Menu

Wednesday, 1 January 2014

Wasomi wagawanyika kuhusu Serikali Tatu




Dar na mikoani: Pendekezo la muundo wa Serikali Tatu lililomo katika Rasimu ya Pili ya Katiba, limewagawa wasomi na wanazuoni katika vyuo vikuu na taasisi mbalimbali za elimu ya juu nchini.
Baadhi ya wasomi waliohojiwa na waandishi wetu jana walisema pendekezo la Serikali Tatu litaimarisha Muungano kwani limezingatia matakwa ya wengi, huku baadhi wakitofautiana na wenzao kwa maelezo hatua hiyo ni kurudi nyuma na kuhatarisha kuvunjika kwa muungano.
Rasimu hiyo ambayo ilikabidhiwa juzi kwa Rais Jakaya Kikwete na Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba inapendekeza muundo wa Serikali Tatu, pendekezo ambalo linamaanisha kurejeshwa kwa Serikali ya Tanganyika.
Mwenyekiti wa Umoja wa Wahadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udomasa), Paul Loisulie alisema: “Vyote vilivyopo katika rasimu hiyo navikubali, lakini bado kuna majadiliano kuhusiana na uraia wa Zanzibar na Tanganyika.”
Alisema mjadala pia unahitajika juu ya gharama za kuendesha Serikali ya Muungano ambayo kwa mujibu wa rasimu ndiyo yenye dhamana ya kusimamia Idara ya Usalama wa Taifa na Polisi.
“Hapa sasa Serikali ya Tanganyika na ya Zanzibar zitabaki na nini kama Usalama na Polisi utakuwa chini ya Muungano?” alihoji.
Hata hivyo, alisema rasimu hiyo ya pili imekidhi kwa kiasi kikubwa mapendekezo ya wananchi... “Tume inahitaji pongezi, suala la Muungano linavuta hisia za watu wengi na litaendelea kuchukua sehemu kubwa ya mjadala, tunaomba Bunge la Katiba nalo lizingatie matakwa ya watu,” alisema Loisulile.
Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (Sua), Dk Mikidadi Muhanga alisema licha ya pendekezo la Serikali Tatu kuwa la wananchi, muundo huo utazidisha gharama za uendeshaji wake.
“Kama nchi tulipaswa kuangalia uhalisia zaidi kuliko utashi wa wananchi. Kutakuwa na mahitaji makubwa ya fedha kwa ajili ya kuendesha Serikali Tatu tofauti na ilivyokuwa kwa Serikali Mbili,” alisema Dk Mikidadi.
Alisema kwa kuzingatia kuwa wananchi wengi wamependa muundo huo, basi wawe tayari kupokea changamoto zake na wasije lalama, wawe wavumilivu wakati watakapoanza kuonja uchungu wa gharama hizo.
Wapendekeza Serikali Moja
Mkuu wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Ushirika na Biashara Moshi (MUCCoBS), Profesa Faustine Bee alisema yangekuwa ni matakwa yake, angependekeza muundo wa Serikali Moja.

No comments:

Post a Comment