Arusha.Watu saba wamefariki dunia papo hapo katika ajali ya barabarani iliyotokea usiku wa kuamkia Januari 5 mwaka huu katika eneo la Mti mmoja, wilayani Monduli.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo na kwamba miili ya marehemu imehifadhiwa katika Hospitali ya Mkoa wa Mount Meru.
Alisema ajali hiyo ilihusisha magari ya mizigo aina ya Scania lililogongana na Mitsubishi Fuso lililokuwa likiendeshwa na Alex Kessy mkazi wa Ngaramtoni wilayani Arumeru.
Alisema Scania lilikuwa linaendeshwa na mtu liyefahamika kwa jina moja la Alfayo, mkazi wa Kimandolu jijini Arusha.
Alisema ajali hiyo ilitokea wakati gari aina ya scania likiwa linatokea Arusha kwenda Makuyuni na Mitsubishi Fuso lilikuwa linatokea Makuyuni kwenda Ngaramtoni na kusababisha vifo vya watu saba.
Aliwataja waliopoteza maisha kuwa ni Petro Henry mkazi wa Unga Limited, dereva wa Scania aliyetambuliwa kwa jina la Alfayo, mama Peter mkazi wa Oldonyosambu, mama Norbert mkazi wa Sakina, Dadala Boya mkazi wa Oldonyosambu, Alex Kessy mkazi wa Ngaramtoni na mama Ngatai mkazi wa Oldonyosambu.
Alisema polisi wanaendelea kufuatilia majina halisi ya marehemu na kuchunguza chanzo cha ajali hiyo.
SOURCE : Gazeti-Mwananchi
No comments:
Post a Comment