Friday, 27 December 2013
MLANGO WA FATAWA :: Je inafaa kuswali na viatu?
JAWABU
Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.
Kuswali na viatu ni jambo linarohusiwa ndani ya Uislamu. Ikiwa viatu vyenyewe vinavaliwa ndani ya nyumba au nje basi inaruhusika mtu kuswalia kwa sharti viatu hivyo viwe twahara na visiwe na najisi. Utwahara wa hapa unaokusudia ni viatu viwe vikavu.
Ushahidi wa hayo ni:
1-Mara moja alikuwa anavivua wakati anaswali na kisha akiendelea na Swalah yake kama alivyosema Abu Sa'iyd Al-Khudriy: "Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) alituswalisha siku moja, na alipokuwa yumo katika Swalah, alivua viatu vyake na akaviweka upande wa kushoto kwake. Watu walipoona hivyo, nao pia wakavua viatu vyao. Alipomaliza kuswali alisema: ((Kwanini mmevu aviatu vyenu?)) Wakajibu: "Tumekuona wewe unavua viatu vyako nasisi pia ndio tukavua viatu vyetu". Akasema: ((Hakika Jibriyl alinijia na kunijulisha kwamba kulikuwa na uchafu)) au kasema (kulikuwa na) kitu cha madhara)). Katika riwaya nyingine ((uchafu/ Najsi)) katika viatu vyangu, kwahiyo nikavivua. Kwa hivyo, mmojawenu anapokuja msikitini, basi atazame viatu vyake. Akiona vina uchafu, au kasema kitu chenye madhara, na (katika riwaya nyingine) najsi, basi avifute kisha aswali navyo)). Abu Daawuud 650, Ibn Khuzaymah na al-Haakim ambao wamekiri kuwa ni Swahiyh na adh-Dhahabiy na an-Nawawiy wamekubali. Ya kwanza imetolewa katika Irwaa. Na Al baaniy ameiweka kama ni hadithi sahihi katika kitabu cha Al SaheehAbi Dawood,605).
2-Na kauli yake Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) iliyopokewa na Abu Salamah Sa‘iyd bin Yaziyd aliyesema: “Nilimuuliza Anas (Radhiya Allaahu ‘anhu): Je, Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akiswali na viatu vyake”. Akasema: “Ndio” (al-Bukhaari, 386; Muslim, 555).
Hadithi za hapo juu zinaonyesha wazi kuwa inafaa ila tuzingatie viatu viwe twahara na visiwe na najisi. Ila tukumbuke haya yalitokea wakati wa Mtume (swalla Allahu alayhi wasallam), wakati ambapo hakukuwa na mazulia wala mabusati msikitini.
SUALI
Je nı ıpı hukumu ya kusalı msıkıtını na vıatu kwa mısıkıtı ambayo ına mazulıa na vyenye kufanana na hıvyo?
JAWABU
Tutalijibu suala hilo kwa kuangalia hukumu mbali mbali zilizotolewa na maulamaa.
1-JAMHURI YA WANAZUONI
Jamhuri ya wazuoni waliulizwa “Nini hukumu ya mtu kusawali na viatu?
Jibu: Mtume swalla Allahu alayhi wasallam aliingia msikitini na viatu na akasali na viatu. Abuu Daud amepokea hadithi ndani ya Sunan yake inayosema : alivyosema Abu Sa'iyd Al-Khudriy: "Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) alituswalisha siku moja, na alipokuwa yumo katika Swalah, alivua viatu vyake na akaviweka upande wakushoto kwake. Watu walipoona hivyo, nao pia wakavua viatu vyao. Alipomaliza kuswali alisema: ((Kwanini mmevua viatu vyenu?)) Wakajibu: "Tumekuona wewe unavua viatu vyako nasisi pia ndio tukavua viatu vyetu". Akasema: ((Hakika Jibriyl alinijia na kunijulisha kwamba kulikuwa na uchafu)) au kasema(kulikuwa na) kitu cha madhara)). Katika riwaya nyingine ((uchafu/ Najsi))katika viatu vyangu, kwahiyo nikavivua. Kwa hivyo, mmoja wenu anapokuja msikitini, basi atazame viatu vyake. Akiona vinauchafu, au kasema kitu chenye madhara, na (katika riwaya nyingine) najsi, basi avifute kisha aswali navyo)). Abu Daawuud 650).
Pia Abu Dawood amepokea kutoka kwa Ya’la ibn Shaddaad ibn Aws kuwa baba yake amesema “Mtume Muhammad (swalla Allahu alayhi wasallam) amesema “Tofautianeni na mayahudi kwani wao huswali bila ya viatu na khofu kwenye miguu yao “
Na pia Abu Dawood amepokea kutoka ‘Amr ibn Shu’ayb, kutoka kwa baba yake, kuwa babu yake amesema:” Nimemuona Mtume (swalla Allahu alayhi wasallam) akiswali na viatu na pia bila ya viatu.” Pia imepokewa na Ibn Majah.
Ila kwa kawaida misikiti ya sasa inamazulia ndani yake. Hivyobasi mmoja wenu atakapoingia msikitini avue viatu vyake, na awe muangalifu ili asilichafue zulia pia asijekuwakera waislamu wengine kutokana na uchafu unaoweza kuingia ndani ya zulia hata kama viatu viko safi.
Fataawa al-Lajnah al-Daa’imah, 6/213, 214
2-SHEIKH ABDALLAH IBN HUMAYD
“Kuruhusiwa huku kusalia na viatu ni kwa ajili ya zama za wakati huo. Ila ikiwa msikiti una mazulia ndani yake, lazima msikiti uwekwe safi hivyo asiingie mmoja wenu na viatu”
(Fataawa Samaahat al-Shaykh ‘Abd-Allaah ibn Humayd, uk. 81)
3-SHEIKH IBN BAAZ
Sheikh Ibn Baaz aliwahi kuulizwa kuhusu kuswali na viatu?
Akajibu :” Kusali na viatu ni jambo mustahab baada ya kuhakikisha viatu ni twahara na havina najisi. Kwa sababu Mtume Muhammad (swalla Allahu alayhi wasallam) amesema “Tofautianeni na mayahudi kwani wao huswali bila ya viatu na khofu kwenye miguu yao “ Ila kuswali bila ya viatu hakuna tatizo kwani pia Mtume (swalla Allahu alayhi wasallam) ameswali bila ya viatu.
Ikiwa msikiti una mazulia ni bora mtu kuvua ili asiliharibu zulia na kuwa chafu au kuwazuia waislamu wengine wasisujudu juu yake. Mwisho wa kunukuu. ( Majmoo’ Fataawa Ibn Baaz).
4-SHEIKH al-ALBAANY
Sheıkh al-Albaany amesema “ Nimewashauri ndugu zetu wa kisalafy wasiwe wenye kutilia mkazo sana juu ya suala hili (kusali na viatu). Kwani kuna tofauti, misikiti ya zama hizi ina mazulia ndani yake tofauti na msikiti wakati wa Mtume Muhammad (swalla Allahu alayhi wasallam). Nikawapa ushahidi mwengine kutoka katika hadithi Mtume (swalla Allahu alayhi wasallam) amewaamrisha maswahaba zake ((Mmoja wenu anaposwali, asiweke viatu vyake upande wa kulia wala kushoto kwake, ambako vitakuwa katika upande wa kulia wa mwenzake, isipokuwa kama kutakuwa hakuna mtu upande wa kushoto, lakini aviweke baina ya miguu yake)). Haya yaliruhusiwa kwa sababu wakati huo hakukuwa na mazulia. Ila misikiti ya sasa ina mazulia ndani yake, je wanawaambia na kuwahimiza waumini kuwa pia inafaa kuweka viatu juu ya mazulia? Hali zote hizo ni sawa. Mwishowakunukuu.
HITIMISHO
Kutoka na ushahidi ulotolewa hapo juu ni bora zaidi muislamu akiswali ndani ya misikiti yenye mazulia avue viatu vyake kwani tumeona maulamaa wakubwa wakubwa nini wameeleza juu ya suala hilo. Hivyo anaetaka kudumisha sunna hii basi aswali kwake na viatu lakini akienda msikitini avueviatu. Ili kuepusha kuleta gharama inayoweza kuepukika. Pia kuswali na viatu kutapelekea misikiti kuwa michafu jambo litakalotuondoshea sifa waumini kwani waislamu ni wasafi na pia itabidi waajiriwe watu ambao kila baada ya swala wasafishe mazulia. Na jengine kubwa zaidi itakuwa unawakera waislamu wenzako kutokana na michanga itokayo ndani ya viatu au vumbi la viatu vilivyo tembelewa kutwa nzima. Pia inawezekana waislamu wasiswali sehemu ulizokanyaga na viatu. Hivyo utajikuta unabeba jukumu jengine kwa Allah. Elimu inataka hekima ndani yake. Vijana tusomeni zaidi na tutangulizeni hekima mbele. Sio kukurupuka tu katika mambo.
Na Allah ni mjuzi zaidi.
Labels:
religions
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Subuhanallah kwan Kati ya suna na mazulia kipi nibola na ikiwa JAMBO furan nisababu ya kuwacha sunna au wajibu je JAMBO hilo litakuwa sahh
ReplyDeleteThank You and I have a tremendous provide: Who Repairs House Foundations remodel old house
ReplyDelete