Sehemu tulipofikia wiki iliyopita
Habari kwa mfalme zikaenda kuwa yule kijana wake aliemchagua kwa ajili ya kujifunza uchawi ana elimu nyengine kabisa sio ile ya uchawi ambayo amemtuma.Kwani amekuwa anatibu watu wenye maradhi mbali mbali kwa kuwaombea dua na wanapona. Mmoja wa washauri wa mfalme alikuwa amezeeka kiasi ya kwamba macho yake hayaoni vizuri. Hivyo basi wakati mfalme anapewa habari kuhusu kijana wake kuwa anatibu watu na mengineyo akasema na mimi tayari nimeshapata dawa. Akaenda kwa yule kijana akaombewa dua akapona na akawa anaona kama kawaida.
Mfalme tayari amekasirika huku akitaka kujua sababu ni ipi hasa inayomfanya
huyu kijana kuwa hivi. Maana amekuwa na elimu ambayo hata yule mchawi wake hana. Hivyo akaamuwa kumwita yule kijana. Yule mchaMungu alimwambia kijana kuwa asije kumtaja kwa mtu yoyote kuwa yeye ndie aliemfundisha ile elimu hata kama atatishiwa kuuliwa.
Wakati kijana yuko mbele ya mfalme akaingia yule mshauri wa mfalme. Mfalme kumuona tu yule mshauri wake anaingia ndani bila ya kuongozwa na wakati alikuwa haoni ikabidi amuulize nani aliekufanya hivi wakati wewe ulikuwa huoni? Yule mshauri wa mfalme akajibu huyu kijana. Ameniombea dua na sasa naona. Kijana akaulizwa na mfalme je wewe unatibu watu? Kijana akajibu sijatibu mtu mimi bali ALLAH (subhanahu wataala) amewatibu. Akaulizwa tena kijana na mfalme je una Mungu asiekuwa mimi? Kijana akajibu Mola wangu na mola wako wewe ni ALLAH. Mfalme akamuuliza tena yule kijana elimu ulionayo sio elimu ya mchawi je umejifunzia wapi hii elimu? Kijana akasema nimejifundisha. Akamuuliza mchawi wake je umemfundisha wewe? Mchawi akasema hapana mimi sijui kabisa kuhusu elimu hii. Mfalme akamwambia kijana nitakutesa mpaka useme umejifunza kutoka wapi. Kijana akawa ameshikilia msimamo wake kuwa amejifunza bila ya kumtaja. Akamtesa vya kumtesa kijana bado hajataja ni nani aliyemfundisha elimu ile mwisho kijana mateso yakamzidi akamtaja yule mchaMungu ambae alimwambia asimtaje. Hivyo basi mwalimu wake mchaMungu akachukuliwa mpaka kwa mfalme. Kijana na mchaMungu wakakuwepo mbele ya mfalme .Akaulizwa mchaMungu je utarudi katika dini ya mfalme au tukutese? MchaMungu akajibu “LAA ILAHA ILLA ALLAH”Mzee hakutetereka na jibu lake hilo akatateswa na jibu lake likawa “LAA ILAHA ILLA ALLAH” Wakachukua msumeno wakamwambia tutakukata vipande viwili au urudi katika dini ya mfalme. MchaMungu akabaki na jibu hilo hilo la LAA ILAHA ILLA ALLAH. Wakachukua msumeno na wakamkata vipande viwili mbele ya yule kijana. Hivyo yule mzee mpaka roho inamtoka neno lake lilikuwa ni LAA ILAHA ILLA ALLAH. Baada ya hapo wakamwambia yule kijana umeona nini kilichotokea kwa mwalimu wako? Na wewe ukikataa utapata mateso kama haya au zaidi ya haya.
Hivyo akaamuru walinzi wake wamshike yule kijana na waende nae katika mlima mrefu wakamuue ikiwa atakataa kurudi katika dini ya mfalme. Walinzi wakatii amri wakaenda nae mpaka kwenye kilele cha mlima mrefu kabisa. Walipofika kule wakamwambia yule kijana”Kubali kurudi katika dini ya mfalme au tutakurusha chini ufe kinyama kabisa” Kijana akawajibu “LAA ILAHA ILLA ALLAH” Wakati wanataka kutupa kijana akanyanyua mikono akaomba dua kwa ALLAH (subhanahu wataala) akasema “Ewe mola wangu nitosheleze kutoakana na hawa kwa unavyoweza” Ghafla jabali likatikisika wakaanguka wale walinzi wa mfalme akabaki peke yake yule kijana. WALLAH huyu kijana alikuwa ni kijana wa maajabu kwani kwa mtu mwengine ambae ameepukana na kifo basi angekimbia tu ila kijana akarudi mwenyewe kwa mfalme. Mfalme akamuuliza wako wapi walinzi wangu? Kijana akajibu Allah amewatosheleza kwa vile anavyoweza wamekufa wote. Mfalme akaamuru akamatwe tena afungwe vizuri na wakamtupe baharini. Walinzi wale wakatengeneza kama dema hivi ili wamtie yule kijana. Ila kabla hawajamuweka katika dema wakamwambia rudi katika dini ya mfalme au tutaenda kukuzamisha. Kijana akaomba tena dua ile ile “Ewe mola wangu nitosheleze kutokana na hawa kwa unavyoweza” Ghafla jahazi likatisika wakaanguka wale walinzi na wakafa hapo hapo. Kijana hakukimbia akarudi tena kwa mfalme. Mfalme kumuona yule kijana akamuuliza tena juu ya wanajeshi wake, akamwambia wamekufa katika bahari. Mfalme sasa akawa anawaza nitamfanya nini huyu kijana maana kila ninachofanya anashinda yeye hafi. Kijana akamwambia yule mfalme “Wewe huwezi kuniua mimi hadi ufate masharti ninayotaka mimi” Mfalme akamwambia niambie hayo masharti yako, mimi muhimu ninachotaka wewe ufe. Kijana akamwambia katika siku fulani wakusanye watu wote katika mji huu katika eneo moja. Watu wote wakae chini na kimya washuhudie tukio hili. Kisha nifunge katika mti. Na baadae unipige mshare. Mfalme akaamrisha wanajeshi wake watangaze kwa watu kuwa siku fulani wote wakuwepo sehemu fulani. Siku ikafika yule kijana akapelekwa pale akafungwa katika mti ili auliwe. Watu wakakusanyika sasa kushuhudia kuuwawa kwa yule kijana. Mfalme ikawa akitaka kumchoma mshare yule kijana mshare haumpati. Mwisho yule kijana akamwambia yule mfalme huwezi kuniua mpaka useme kile nitakachokwambia mimi useme. Mfalme akasema niambie nitasema chochote mimi alimradi nikuue tu wewe usikuwepo dunian. Kijana akamwambia pale unapouvuta upinde wako ili kuniua sema “BISMILLAHI RABBAL GHULAAM (KWA JINA LA MWENYEZIMUNGU MOLA WA KIJANA HUYU”Ukisema vyengine huwezi kuniua. Pia uyaseme maneno hayo wakusikie watu wote waliokusanyika. Naam mfalme akasema vile vile na akarusha mshare na ule mshare ukaenda kumchoma yule kijana na yule kijana akafa. Watu waliokusanyika wakasema huyu mfalme alijaribu kila njia kumuua huyu kijana lakini ameshindwa kwa nini alipomtaja huyu Allah akafa kijana? Bila ya shaka huyu Allah ndio mungu. Watu waliokusanyika sasa wakaanza kusema LAA ILAHA ILLA ALLAH. Watu wamji mzima wakaingia katika Uislamu. Kifo cha kijana yule kimesababisha umma mzima ulokusanyika kuingia katika Uislamu. Mfalme, walinzi wake na mawaziri wakaogopa kuwa wailsmau. Hivyo basi mfalme alipoona kuwa mji mzima umekuwa waislamu, wale washauri wake wakamwambia kuwa tuchimbe handaki kubwa ili tuwachome wale wote waliosema kuwa wewe sio mungu.Likachimbwa handaki kubwa kabisa likawashwa moto na moto ukakolea kikweli kikweli. Sasa ikawa watu wanasogezwa unaulizwa chagua dini ya mfalme au tukutupe katika moto. Watu wengi wakakubali bora watupwe katika moto kwa sababu ya Allah. Hivyo wengi wao wakachomwa katika handaki lile lenye moto. Mwishoni kabisa akaja mama mmoja ambae ana mtoto mchanga. Akasema mimi nitajitupa ila huyu mtoto ana dhambi gani? Lakini Allah akampa kauli yule mtoto mdogo azungumze mtoto akasema: “ Ewe mama subiri wewe upo katika haki” Mama aliposikia anahamasishwa na mtoto wake pale pale akajitupa katika moto.Kifo cha kijana kimesababisha haya yote.
Kisa hiki pia kimeelezewa na Imam Muslim.
In shaa Allah tutaendelea na darsa ya tafsiri ya Suratul Buruuj Alhamis ijayo.Tunauomba ALLAH atujaalie miongoni mwa wale watakaoukuwa na ufahamu wa Quraan na kuifanyia kazi.Aaamin.ALLAH NI MJUZI ZAIDI.
No comments:
Post a Comment