Drop Down MenusCSS Drop Down MenuPure CSS Dropdown Menu

Friday, 27 December 2013

MAKALA YA IJUMAA 24 /Swafar /1435 H :: KUJIFANANISHA NA JINSIA TOFAUTI NAWE

Kila sifa njema zinamstahikia Allah (subuhanahu wa taala) Muumba wa vyote vilivyoma ardhini na mbinguni na baina yao, kisha akaviwekea utaratibu maalum wa kuendesha maisha yao. Sala na salamu zimuendee Mtume wetu Muhammad (swalla Allahu alaihi wa sallam).

Ndugu wa kiislamu, Allah (subuhanahu wa taala) amewalani wanawake wanaojifananisha kiume na wanaume wanaojifananisha kike, na ndio maana ikawa ni katika madhambi makubwa sabini. Mfano wa kujifananisha ni kama vile: Kuzungumza, kutembea, kuvaa mavazi; na kwa wanawake, kumpenda mwanamke mwengine kama wanaume kwa ajili ya
machafu wanawake kwa wanawake (Lesbians), na kwa wanaume, ni kuingiliana wanaume kwa wanaume (Homosexuals). Kutokana na maumbile, Allah (subuhanahu wa taala) ameumba wanaume na wanawake, na tabia zao na mavazi yao na msemo wao ni tofauti kabisa, lakini ikiwa mwanamume atajifananisha kuwa sawa na mwanamke au mwanamke kuwa sawa na mwanamume, basi watakuwa wamezibadili wao wenyewe taratibu walizopangiwa na kuwekewa na Mola wao, na kwa hivyo watakuwa wametenda dhambi kubwa. Mtume (swalla Allahu alaihi wa sallam) amesema katika Hadithi iliyotolewa na AL-Bukhari,
“لَعَنَ الله الْمُتَشَبِّهَاتِ مِنَ النِّسَاءِ بِالرِّجَالِ وَالْمُتَشَبِّهِينَ مِنَ الرِّجَالِ بِالنِّسَاءِ’’
“Wamelaaniwa na Mwenyezi Mungu wanawake wanaojifananisha kiume na wanaume wanaojifananisha kike.”
Pia Mtume (swalla Allahu alaihi wa sallam) amesema katika Hadithi nyingine iliyopokelewa na Abu Daud kutoka kwa Ibn Abbas (radhi za Allah ziwe juu yake),
“لَعَنَ اللَّه الْمُخَنَّثِينَ مِنَ الرِّجَالِ وَالْمُتَرَجِّلاتِ مِنَ النِّسَاءِ’’
“Mwenyezi Mungu amewalani wanaume wanaojifananisha kike na wanawake wanaojifananisha kiume.”
Vile vile Mtume (swalla Allahu alaihi wa sallam) amesema katika Hadithi iliyopokelewa na AL-Bukhari kutoka kwavAbu Huraira (radhi za Allah ziwe juu yake)
“لَعَنَ اللَّه المرأة تلبس لبسة الرِّجَالِ والرِّجَالِ يلبس لبسة المرأة’’
“Mwenyezi Mungu amemlaani mwanamke anaevaa mavazi ya kiume na mwanamume anaevaa mavazi ya kike.”
Na ikiwa mwanamke kaolewa, na mumewe yuko radhi na kitendo hiki na hataki kumzuia kwa tabia hii, huwa naye pia anashiriki kwa sababu ya kutokana na amri ya Allah (subuhanahu wa taala) katika Suratul Tahriim aya ya 6,
“يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا قُوا أَنفُسَكُمْ وَأَهْلِيكُمْ نَارًا وَقُودُهَا النَّاسُ وَالْحِجَارَةُ...
“Enyi mlioamini! Jiokoeni nafsi zenu na watu wenu, na Moto ambao kuni zake ni watu na mawe...”
Mwanamume anabeba masuulia makubwa ya kumfundisha dini mkewe na wanawe ili wamtii Allah (subuhanahu wa taala) na kuwazuia kufanya maasi. Na asipofanya hivyo ataulizwa kesho siku ya Kiyama na atashindwa kujibu. Na pia mke anabeba masuulia ya ulinzi wa nyumba ya mumewe na watoto wake. Mtume (swalla Allahu alaihi wa sallam) amesema katika Hadithi iliyopokelewa na AL-Bukhari na Muslim na kutolewa na Ibn `Umar (radhi za Allah ziwe juu yake),
“كُلُّكُمْ رَاعٍ وَكُلُّكُمْ مَسْئُولٌ عن رعيته . الرَّجُلُ رَاعٍ في أَهْلِهِ وَمَسْئُولٌ عنهم يوم القيامة’’
“Nyinyi nyote ni walinzi na nyinyi nyote mtaulizwa (kila mmoja wenu) kwa ulinzi wake. Mwanamume ni mlinzi kwa watu wake (mkewe na wanawe) na ataulizwa juu yao siku ya Kiyama.”
Pia Mtume (swalla Allahu alaihi wa sallam) amesema: Kuwatii wanawake kwa maasi ni kuangamizwa kwa wanaume, katika Hadithi iliyopokelewa na Muslim na kutolewa na Abu Huraira (radhi za Allah ziwe juu yake),
“ألآ هَلَكَتْ الرِّجَالُ حين أطَاعُوا النِّسَاء’’
“Kwa kweli, wanaume wanaangamia wakati wanapowatii wanawake (kwa maasi).”

Na pia Uislamu umewaharamishia wanawake kuvaa nguo ambazo hazifuniki miili yao vizuri. Na kuvaa zile nguo za kubana zinazoonyesha maumbile ya maungo yao na hasa zile sehemu zinazowavutia wanaume ndizo zenye kuleta fitina kubwa. Mtume (swalla Allahu alaihi wa sallam) kafananisha uchanaji wa nywele zao wanawake hao kama nundu ya ngamia. Na huu ni miongoni mwa miujiza mikubwa ya Mtume (swalla Allahu alaihi wa sallam) kwani kama vile aliwaona wanawake wa sasa mavazi yao na uchanaji wao, ambapo zama zake hapakuwepo na wanawake wa aina hii. Mtume (swalla Allahu alaihi wa sallam) akaongezea kwa kusema: Wanawake wa aina hii hawataingia Peponi, katika Hadithi iliyopokelewa na Muslim na kutolewa na Abu Huraira (radhi za Allah ziwe juu yake) Mtume anasema:
“نِسَاءٌ كَاسِيَاتٌ عَارِيَاتٌ مُمِيلاتٌ مَائِلاتٌ ، رُءُوسُهُنَّ كَأَسْنِمَةِ الْبُخْتِ الْمَائِلَةِ ، لا يَدْخُلْنَ الْجَنَّةَ وَلا يَجِدْنَ رِيحَهَا وَإِنَّ رِيحَهَا لَيُوجَدُ مِنْ مَسِيرَةِ كَذَا وَكَذَا’’
“Wanawake wamevaa mavazi ya uchi (yaani ingawa wamevaa nguo lakini wako uchi, kwa sababu ya nguo zao nyepesi zinaonyesha miili yao, na nguo za kubana zinazoonyesha umbile la maungo yao) wameelemea kuinama (kwa kupenda kuvaa nguo za kutojisitiri), (kwa namna walivyochana nywele zao) vichwa vyao (vimefanana) kama nundu za ngamia vimeinama, hawataingia Peponi wala hawatapata harufu yake. Na hakika harufu yake inapatikana kutoka umbali wa hivi na hivi.”

Hivyo ndugu wa kiislamu ni juu yetu kuchunga amri, mipaka na taratibu alizotuekea Allah (subuhanahu wa taala) kwani kufanya hivyo ndio kutatupelekea kupata salama hapa duniani na kesho Akhera. Laa tukiamua kufanya kiburi na kujivuna baada ya kufikiwa na maonyo yatokayo kwa Allah, khasara ya milele itatukumba na Akhera tutakuja kufufuliwa hali ni vipofu kama Allah (subuhanahu wa taala) anavyosema: “Na atakaye jiepusha na mawaidha yangu, basi kwa yakini atapata maisha yenye dhiki, na Siku ya Kiyama tutamfufua hali ya kuwa kipofu. Aseme: Ewe Mola wangu Mlezi! Mbona umenifufua kipofu, nami nilikuwa nikiona? (Mwenyezi Mungu) atasema: Ndivyo vivyo hivyo. Zilikufikia ishara zetu, nawe ukazisahau; na kadhaalika leo unasahauliwa.” [SURAT TWAHA (20): 124-126]

Allah atujaalie tuwache mabaya tunayoyafanya kwa siri na kwa dhahiri na atuwafiqishe kufanya toba ya kweli atakayoiridhia na atuwezeshe kupata radhi zake. Amin.

No comments:

Post a Comment