Drop Down MenusCSS Drop Down MenuPure CSS Dropdown Menu

Friday, 3 January 2014

Mzozo wa mapenzi waua Mbeya, Singida

 MKAZI wa Kijiji cha Mwasutianga, Kata ya Irisya, wilayani  Ikungi, Singida, Mwanahamisi Mwangu (72), amekufa baada ya kupigwa mateke na ngumi na mumewe, Salehe Mohammed (75) kutokana na ugomvi baina ya marehemu na mke mwenzie wakigombea ndoo ya maji.
Tukio hilo limetokea Januari mosi mwaka huu, saa 7 mchana wakati wakiwa shambani wakipanda mazao.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Singida, Geofrey Kamwela, alisema siku ya tukio Mwanahamisi alikuwa shambani na mumewe pamoja na mkewe mdogo, Fatuma Ramadhani (55). Walikuwa wakipanda mtama, lakini ghafla ulizuka ugomvi wa kugombea ndoo iliyokuwa na maji.
Alisema katika ugomvi huo kila mmoja akidai  ndoo hiyo ni mali yake, ndipo mume wao alipoamua kuingilia ugomvi huo.
“Mtuhumiwa mzee Salehe katika ugomvi huo alikuwa upande wa mke mdogo ndipo alianza kumpiga mateke na ngumi mkewe mkubwa Mwanahamisi na kusababisha kifo chake papo hapo,” alisema Kamwela.
Alisema polisi wanamshikilia mtuhumiwa na anatarajiwa kufikishwa mahakamani muda wowote baada ya upelelezi kukamilika.
Katika tukio jingine, Shauri Samwel (22) mkazi wa Kijiji cha Tyeme, wilayani Iramba, amefariki dunia baada ya kunywa vidonge vya kuhifadhia nafaka.
Alisema tukio hilo lilitokea Desemba 31 mwaka jana, saa 12 jioni katika zahanati ya Kijiji cha Tyeme wakati Shauri akiendelea kupatiwa matibabu.
Kamanda Kamwela alisema chanzo cha kunywa vidogo hivyo  ni hofu aliyokuwa nayo Shauri kutokana na kumtia ujauzito binamu yake.
Katika tukio jingine, watu wawili wamefariki dunia katika matukio tofauti jijini hapa  likiwemo la mwanamke mkazi wa Inyara, Huruma Laiton (20) ambaye aliuawa kwa kipigo kutoka kwa mumewe baada ya kumfumania akiwa anafanya mapenzi na binamu yake.
Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Kamishna Msaidizi wa Polisi, Ahmed Msangi, alisema  mwanamke huyo aliuawa juzi majira ya saa 11:00 jioni nyumbani kwake katika Kijiji cha Inyara.
Alisema tukio hilo la kinyama linadaiwa kufanywa na mume wa marehemu, Ezekiel Mwakabenga (21) ambaye anadaiwa kumpiga mkewe kwa kutumia ngumi, fimbo na mateke na kumsababishia majeraha makubwa ambapo alikimbizwa katika hospitali ya rufaa jijini hapa na kufariki dunia akiwa anapata matibabu.
Msangi alisema Mwakabenga ambaye ni mfanyabiashara alimkuta mkewe akifanya mapenzi na binamu yake ndani ya nyumba yao, kitendo ambacho kilimchukiza, hivyo kuamua kumpiga.
Mwilii wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya Rufaa Mbeya na mtuhumiwa anashikiliwa na polisi.
Katika tukio jingine la mauaji lilitokea katika Kijiji cha Nsalaga, Tarafa ya Iyunga ambapo  fundi muashi,  Christopher Myamba (20) ameuawa kwa kuchomwa na kisu shingoni baada ya kutokea mzozo na marafiki zake wakati wakitoka kunywa pombe kilabuni.
Tukio hilo limetokea Januari mosi mwaka huu majira ya saa 7:00 kamili mchana  katika eneo la Itezi Mashariki, jijini Mbeya.
Alisema kuwa marehemu alichomwa na kisu shingoni na mtu aliyefahamika kwa jina moja la Ndele baada ya kutokea mzozo wa marafiki hao.
SOURCE : Tanzania Daima

No comments:

Post a Comment