
Wanawake wa Harakati ya Wanawake Dhidi ya Mapinduzi ya Kijeshi nchini Misri, wamefanya maandamano kupinga kimya cha Shirika la Kutetea Haki za Binaadamu nchi humo katika kukabiliana na jinai za majeshi ya serikali dhidi ya raia. Harakati hiyo imesema kuwa imeitisha maandamano hayo, kutetea heshima na uhuru wa nchi na kusisitizia wajibu wa
kurejeshwa utawala wa kisheria uliochaguliwa na wananchi. Aidha kwa mujibu wa harakati hiyo, wanawake hao wameandamana mbele ya baraza la haki za binaadamu nchini Misri, kulalamikia kimya cha shirika hilo katika kukabiliana na unyanyasaji dhidi ya wanawake unaofanywa na askari wa serikali. Kwa upande mwingine makundi yanayopinga mapinduzi ya kijeshi nchini humo, yametangaza azma yao ya kuanzisha maandamano makubwa katika medani maarufu ya Tahrir na kubakia hapo ili kuzidi kuishinikiza serikali ya hivi sasa mpito. Hayo yamesemwa na baadhi ya viongozi wa mirengo tofauti nchini Misri ikiwemo Harakati ya Wanafunzi Dhidi ya Mapinduzi ya Kijeshi na kwamba maandamano hayo yatafanyika hii leo katika medani hiyo ambapo watapiga kambi katika kuishinikiza serikali ya kijeshi kujiuzulu. Maandamano hayo yatafanyika katika kupinga pia hujuma za vikosi vya usalama dhidi ya wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Kiislamu cha al-Azhar nchini humo. Aidha maandamano hayo yanaitishwa katika hali ambayo, serikali ya mpito ya nchi hiyo hivi karibuni ilipasisha sheria ya kupiga marufuku maandamano ambapo kwa mujibu wa sheria hiyo, kutatolewa adhabu mbalimbali za vifungo ikiwemo kulipa fidia kwa watu watakao kwenda kinyume na sheria hiyo.
SOURCE : Iran Swahili
No comments:
Post a Comment